Ujumbe wa ubalozi wa China ukiongozwa na Balozi wake nchini Tanzania Lou You Qing (kulia), uliofika nyumbani kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad huko Mbweni kwa ajili ya kujitambulisha na kubadilishana mawazo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na balozi wa China nchini Tanzania Lou You Qing, wakati ujumbe wa ubalozi huo ulipofika nyumbani kwake Mbweni kwa ajili ya kujitambulisha na kubadilishana mawazo. Katikati ni mkalimani wa lugha ya Kichina na Kiingereza Fang Wang.
Picha na Salmin Said-Ofisi Ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar 
---
China imesema itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo zikiwemo elimu, afya, kilimo na utafiti.

Balozi wa China nchini Tanzania Bw. Lou You Qing ambaye aliongoza ujumbe wa ubalozi huo, ameeleza hayo alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.

Balozi Qing na ujumbe wake walifika nyumbani kwa Makamu wa Kwanza wa Rais huko Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, kwa ajili ya kujitambulisha rasmi na kubadilishana mawazo juu ya maeneo tofauti ambayo China na Zanzibar zinaweza kushirikiana.
Amesema China iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika kuendeleza kilimo cha mpunga pamoja na ujenzi wa miundombinu ya maendeleo, ikiwa ni pamoja kuyaalika makampuni ya kichina kwa ajili ya kuangalia namna yanavyoweza kusaidia katika ujenzi wa bandari mpya ya kibiashara Zanzibar.

Balozi Qing amesema China na Zanzibar zina historia ya muda mrefu katika nyanja mbali mbali zikiwemo siasa na uchumi, na kutaka mashirikiano hayo yaendelezwe kwa maslahi ya pande hizo mbili.

Amefahamisha kuwa uhusiano huo wa kunufaishana, sana unaonekana kukua kwa kasi kubwa kutokana na kuwepo na mawasiliano ya karibu miongoni mwa wananchi wa pande hizo mbili, na kwamba hali hiyo itahamasisha kasi ya maendeleo hapa Zanzibar.

Amesifu juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miundominu ya kiuchumi, sambamba na kudumisha hali ya amani, mambo ambayo ni muhimu katika kuchochea maendeleo.

Amesema hatua hizo muhimu, zinaweza kuisadia Zanzibar kupiga hatua kubwa za maendeleo ikizingatiwa kuwa inazo rasilimali muhimu zikiwemo historia, utamaduni, bahari na jiografia ya visiwa vya Zanzibar ambavyo ni muhimu katika kukuza sekta ya utalii.

Amebainisha kuwa kihistoria China ilikuwa nchi maskini, lakini imeweza kupiga hatua kubwa za maendeleo kutokana na mipango na mikakati imara iliyojiwekea ambapo Zanzibar inaweza kujifunza na kukuza uchumi wake.

Nae Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar inayo mengi ya kujifunza kutoka kwa marifiki zao wa China katika jitihada zake za kujikwamua kiuchumi.

Amesema hatua ya Serikali ya China kukubali kuwapeleka mawaziri na maofisa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenda kujifunza nchini China ni muhimu katika kufikia malengo yake iliyojiwekea.

Maalim Seif amepongeza mchango wa Serikali ya China katika kukuza maendeleo ya Zanzibar ambapo nchi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya sekta mbali mbali zikiwemo elimu, afya na Michezo.

Amesema msisitizo wa mashirikiano kwa sasa unapaswa kuekezwa katika sekta za viwanda vidogovidogo, kilimo, utafiti na utalii, ambapo China ina uzoefu mkubwa katika nyanja hizo.

Amesema Zanzibar ambayo inakabiliwa na tatizo la uhaba wa ardhi, inajipanga kuendeleza sekta hizo za kiuchumi hasa kilimo cha umwagiliaji ambacho kinaweza kuinufaisha Zanzibar na hatimaye kupunguza utegemezi wa chakula kutoka nchi nyengine.

Sambamba na hilo Maalim Seif amesema serikali inajipanga kutekeleza mpango wake wa kujenga bandari kubwa ya kibiashara katika eneo la Mpigaduri, na kuiomba China kuangalia uwezekano wa kusaidia utekelezaji wa mpango huo.

Amesema kufanikiwa kwa mpango huo, kutairejeshea Zanzibar hadhi yake ya kuwa kituo kikuu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo meli kubwa za mizigo na kitalii zitaweza kufunga gati na kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao bila usumbufu.

Amefahamisha kuwa inawezekana kwa Zanzibar kujikwamua kiuchumi, kwa kutumia uzoefu wa China ambayo katika kipindi cha miaka 40 iliyopita ilikuwa nchi maskini na sasa uchumi wake unaendelea kukua kwa kasi kubwa kuelekea kutawala uchumi wa dunia.
 
Na
Na Hassan Hamad
Ofisi Ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. inafurahisha kuona urafiki wa Tanzania na China kuendelea kukuwa kwa kiasi kikubwa, ila cha kusikitisha ni kuwa bado tuna concept kwamba someone is there to help us....wachina walikuwa masikina ila kujikomboa imetokana na juhudi zao wenyewe kwenye sector zote, sasa nyumbani sijui tutashindwa nini, kama tukiamua kuchugua strategic ya china basi tuamue kubadilisha mfumo wa nchi, kuondoka kwenye democracy kwani ndo inayoimaliza nchi yetu,..win win policy ya china kwa Africa nayo ni strategic tosha kwa kuendeleza uchumi wa china kwani nyumbani tunanufaka ila sio kama tungeamua kujitoa wenyewe kwenywe umasikini..

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...