Mei 15, 2012
 
ASPIRE KUANZA KUSAKA VIPAJI MEI 21
Mchakato wa kusaka vipaji kwa chipukizi wenye umri chini ya miaka 14 kupitia mpango wa kukuza vipaji wa Aspire Football Dream ambao uko chini ya Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) utafanyika kuanzia Mei 21 mwaka huu.
Vituo vitakavyohusika ambavyo kila kimoja kinatakiwa kuwa na watoto wasiopungua 176 na tarahe ya kufanyika mchakato huo kwenye mabano chini mng’amua vipaji (scout) kutoka Hispania ni Morogoro (Mei 21 mwaka huu saa 3 asubuhi) na Bagamoyo mkoani Pwani (Mei 21 mwaka huu saa 8 mchana).
Vingine ni Kawe, Dar es Salaam (Mei 22 mwaka huu saa 3 asubuhi), Makongo, Dar es Salaam (Mei 22 mwaka huu saa 8 mchana) na Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam (Mei 26 mwaka huu saa 9 mchana).
 
Mpango wa Aspire Football Dream unafadhiliwa na Mtoto wa Mfalme wa Qatar katika nchi 16 duniani kwa Tanzania una jumla ya vituo 14. Vituo vingine ni Kigamboni, Tandika, Ukonga, Kitunda, Mbagala, Magomeni na Tabata.
 
Watoto watakaochaguliwa katika mchakato huo watakwenda katika mchakato mwingine kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki utakaofanyika jijini Nairobi, Kenya.
 
Watakaofuzu kutoka hapo ndiyo watakaokwenda kwenye vituo vya kuendeleza vipaji (centre of excellence) vya Aspire Football Dreams. Aspire ina vituo viwili vya kuendeleza vipaji ambavyo viko Doha, Qatar na Dakar, Senegal.
 
TWIGA STARS KUJIPIMA KWA BANYANA BANYANA
Timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) inatarajia kucheza mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya Afrika Kusini (Banyana Banyana) itakayofanyika Mei 20 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Twiga Stars inayojiandaa kwa mechi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Ethiopia imeingia tena kambini jana (Mei 14 mwaka huu) kujiwinda kwa mechi hiyo itakayochezwa Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa.
 
Banyana Banyana pia iko katika kinyang’anyiro cha kutafuta tiketi ya Fainali za Nane za AWC ambapo katika raundi hii ya pili imepangiwa Zambia na itaanzia mechi hiyo ugenini jijini Lusaka.
 
Mei 12 mwaka huu Twiga Stars ilicheza mechi ya kimataifa ya kujipima nguvu dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors) iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kambi ya timu iko Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Ruvu mkoani Pwani.
 
Naye Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa katika kuimarisha kikosi chake kabla ya mechi ya Jumapili dhidi ya Banyana Banyana amemwita tena kikosi mshambuliaji mkongwe Esther Chabruma.
 
Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Rwanda kuchezesha mechi hiyo ya AWC kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Ethiopia.
 
Waamuzi hao ni Angelique Tuyishime atakayepuliza filimbi wakati waamuzi wasaidizi ni Sandrine Murangwa, Speciose Nyinawabari na Salma Mukansanga. Kamishna wa mchezo huo wa kwanza ni Catherine Adipo kutoka Uganda.
 
Mechi ya marudiano itachezwa Dar es Salaam wiki mbili baadaye ambapo mshindi atapata tiketi ya kucheza Fainali za Nane za AWC zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
 
WATUNISIA KUICHEZESHA STARS ABIDJAN
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeteua waamuzi kutoka Tunisia na Misri kuchezesha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia hatua ya makundi kati ya Taifa Stars na Ivory Coast itakayochezwa Juni 2 mwaka huu jijini Abidjan.
 
Mwamuzi atakuwa Slim Jedidi wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Bechir Hassani, wote kutoka Tunisia. Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Sherif Hassan kutoka Misri. Mwamuzi wa akiba ni Youssef Essrayri pia kutoka Tunisia.
 
Mtathmini wa waamuzi (referee assessor) ni Rachid Medjiba kutoka Algeria wakati Kamishna wa pambano hilo atakuwa Saleh Issa Mahamat kutoka Chad.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 15, 2012

    Huu ndio utani usiokubalika.

    Unatafuta vipaji Morogoro, Pwani na Dar es salam tu. Morogoro kituo kimoja, Pwani kituo kimoja vingine vyote DMS. Hivi nyie TFF munafikiri au munawaza?

    Ushauri wangu mpango kama huu ulifaa ufanywe kwa mikoa yote ili kupata vipaji vingi zaidi sio kwa Aspire programme tu bali hata kwa mipango mingine.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...