Na Sultani Kipingo
Mnamo mwaka 1960 wapiga picha wa kujitegemea huko Italy walijipatia umaarufu mkubwa kutokana na filamu moja iliyokuwa mashuhuri duniani iliyoenda kwa jina la La Dolce Vita (“Maisha Matamu” kwa Kitaliani)  iliyotengenezwa na Producer Federico Fellini wa huko huko Italy.

Hadhithi ya filamu hiyo ya La Dolce Vita inamhusu mwanahabari mchunguzi aliyeitwa Marcello (muigizaji akiwa Marcello Mastroianni) na mpiga picha wake aliyeitwa Paparazzo (muigizaji Walter Santesso). Ingawa bado kuna ubishi wa maana ya jina “Paparazzo”, lakini mfanano wake na jina la mbu mkubwa aitwaye Papataceo kwa lugha ya Kitaliani, ilileta maana kwa kulinganisha maneno ya producer Fellini mwenyewe kwenye taarifa aliyotoa wakati huo.

“Jina Paparazzo kwangu mimi ni kama mbu  anayeruka huku na kule akitafuna watu walio kwenye starehe zao”, alisema Fellini, na kuachia mchoro wa aina ya mtu asiye na mifupa (angalia picha hapo juu kulia) akiwa ameshika kamera ambayo flashi yake inawaka, akimaanisha kwamba paparazzi, kama walivyo mbu, ni wadudu wasumbufu.

Baada ya filamu ya La Dolce Vita kuzinduliwa huko Italy, neno “Papaparazzi likawa linafananishwa na wapiga picha za udaku waliokuwa wakiwinda nyota mbalimbali wa filamu na watu maarufu na kuwaanika magazetini.  Hata hivyo, Fellini alisema yeye hakuwa anawaiga hao wapiga picha za udaku, bali alidai yeye anachofanya ni kuyaingiza magazeti katika filamu, wakati stori zake zilizohusu maisha ya kuponda raha wanayoishi nyota wa filamu ziliuza sana magazeti ya udaku.

Hapana shaka kwamba kuingia kwa neno Paparazzi katika lugha ya Kiingereza kunatokana na hiyo filamu ya La Dolce Vita, pale ilipozinduliwa nchini Marekani huo  mwaka 1961. Na lilikuwa ni jarida maarufu la Time Magazine lililowezesha jina hilo la Paparazzi kupata umaarufu na kuwaganda wapiga picha wa kujitegemea waliokuwa wakisaka habari za udaku za nyota wa filamu.

 Makala ya jarida hilo iliyokuwa na kichwa cha habari cha “Paparazzi on the Prowl” (yaani paparazzi mawindoni), pamoja na picha ya wapiga picha kibao waliokuwa wamezuia gari la Binti Mfalme mmoja aliyekuwa ziarani Rome, ndiyo vilivyokoleza moto.

Makala hiyo ilikuwa inazungumzia jinsi kundi la wapiga picha wa kujitegemea walivyokuwa kama mbwa mwitu mawindoni, wakipita huku na kule kuwinda watu wenye majina makubwa katika jamii, kuwapiga picha wakipinda raha  na kuwaanika kwenye magazeti ya udaku. 
Paparazzi wa Italy wakiwa kazini...


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...