VIONGOZI na watendaji mkoani Pwani wametakiwa kuhakikisha kuwa miradi
yote ya maendeleo inayozinduliwa katika kipindi cha mbio za mwenge iwe
endelevu ili iwasaidie wananchi na si kwa ajili ya mbio hizo.
Baadhi ya miradi imeonekana kuzinduliwa na viongozi wa mbio za mwenge
lakini baada ya muda inakufa jambo ambalo si malengo ya miradi hiyo
ambayo imekuwa mkombozi kwa wananchi katika kutatua changamoto za
kupata huduma za kijamii.
Hayo yamesemwa na kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa Rachel Kasanda
kwenye kijiji cha Bungu wakati wa kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi
wa stendi ya mabasi ya Ikwiriri wilayani Rufiji mkoani humo.
Kasanda amesema kuwa miradi hiyo inapaswa kuwa endelevu ili jamii
iweze kunufaika na si kuwa ya muda kwa ajili ya mwenge kwani hiyo ni
michango ya wananchi, wahisani na serikali hivyo lazima iwe na
manufaa.
Amesema kuwa Viongozi wanapaswa kuhakikisha kuwa miradi hiyo inafanya
kazi baada ya kuzinduliwa kwa kuwa endelevu na kutoa matunda ambayo
yanatarajiwa na wananchi kutokana na ujenzi wake.
Amesema kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa wakifanya miradi hiyo kwa
muda tu ambapo ikishazinduliwa inaachwa hapo hapo pasipo kuendelezwa
na kusababisha kufa jambo ambalo halipaswi kuendelea kufumbiwa macho.
Aidha viongozi na watendaji ndiyo watu wa kuwaonyesha njia wananchi
kwa hivyo wanapaswa kuhakikisha miradi hiyo inakuwa na mafanikio kwa
wananchi ili kuwaondolea changamoto za upatikanaji wa huduma za
kijamii.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Nurdin Babu
amesema kuwa yeye kama kiongozi kwa kushirikiana na watendaji,
viongozi na wananchi watahakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu ili
iwe na manufaa kwa wananchi.
Babu amesema kuwa wamejipanga kuhakikisha miradi hiyo inaleta manufaa
kwa walengwa ambao ni wananchi kwani wamekuwa na changamoto nyingi
ambazo zinatatuliwa hatua kwa hatua kwa kuwashirikisha wadau wa
maendeleo. Mbio hizo za mwenge leo zitakuwa wilaya ya Kibaha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...