Kinachopita ni chake, hata kama si cha kwake,
Chochote kwake ni chake, hata kama cha mwenzake,
Ukicheka usicheke, akikipenda ni chake,
Yeye chake ni cha kwake, cha kwake si cha wenzake!


Kikipendeza ni chake, chake yeye chakwake,
Ukikiona kileke, usikitamani chake,
Macho mbele yapeleke, usigeuzie kwake, 
Yeye chake ni cha kwake, cha kwake si cha wenzake!


Kiwe kitamu cha kwake, na vitamu vya wenzake
Vyote kwake ni vyake, ati yeye haki yake, 
Ugonjwa wake ni wake, tiba ati vya wenzake!


Yeye chake ni cha kwake, cha kwake si cha wenzake!

Kina umbo uzuri chake, chake yeye peke yake,
Mara akishike shike, kuringishia wenzake, 
Atakupiga mateke, ukikigusa cha kwake!
Yeye chake ni cha kwake, cha kwake si cha wenzake!


Vya wanyonge ni vyake, na vya matajiri vya kwake, 
Si haramu huko kwake, vikizuka anga zake,
Toka Pemba Chakechake, hadi Kigoma Isike, 
Yeye chake ni cha kwake, cha kwake si cha wenzake!


Kama vya wenzake vyake, halali kula vya kwake, 
Haki haiwi ya kwake, kama siyo ya wenzake,
Akivila vya wenzake, vitaliwa na vya kwake, 
Yeye chake ni cha kwake, cha kwake ni cha wenzake!


Na. M. M. Mwanakijiji 
(Sauti ya Kijiji)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. CHAKE NI CHAKE (TAHADHARI)

    Kila kipitacho chake, cha kwake si cha wenzake,
    Yu radhi rusha mateke, kwacho chake simpoke,
    Cha watu mpeke peke, kibindoni tia chake,
    Cha kwake si cha wenzake, hadhari na mtu huyo!

    Hafai kuwa rafiki, tena mbali muepuke,
    Chaa wenziwe habanduki, tena mbele ajiweke,
    Kutowa chake hataki, tena mbio enda kwake,
    Cha kwake si cha wenzake, hadhari na mtu huyo!

    Cha weziwe huvinjari, akasifu ladha yake,
    Chake akawa msiri, hufaidi peke yake,
    Pembeni akawanyari, cheka kwa jeuri zake,
    Cha kwake si cha wenzake, hadhari na mtu huyo!

    Chake sifia mororo, kizuri cha peke yake,
    Dai hakina kasoro, kifumbata ndani mwake,
    Kimya na kiza totoro, havinjari peke yake,
    Cha kwake si cha wenzake, hadhari na mtu huyo!

    Cha wenziwe muflisi, humtoka macho yake,
    Hakipi hata nafasi, radhi vunja mambo yake,
    Kisha khitimisha basi, mbio jibanza na chake,
    Cha kwake si cha wenzake, hadhari na mtu huyo!

    Kutenda sitendwe yeye, mbiu ya mgambo kwake,
    Awatendee wenziye, burudani roho yake
    Cha kwake mmuwachiye, wenziwe mmuwalike,
    Cha kwake si cha wenzake, hadhari na mtu huyo!

    H.K.


    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...