Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la Polisi mkoani Pwani limewataka madereva kuwa makini waendeshapo magari na kuacha matumizi ya vilevi ili kuepukana na ajali zisizo za lazima ambazo zinaweza zikajitokeza wakati wa kipindi cha sikukuu ya Eid el Fitr. 

Pia limewataka wanafamilia kutotoka wote majumbani bila ya kuacha watu au kutoa taarifa kwa majirani ili kuepuka wizi na uhalifu unaoweza kujitokeza wakati wa sikukuu.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani humo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP) Ulrich Matei alisema kuwa baadhi ya madereva wamekuwa wakitumia vilevi wakati wa kiendesha magari jambo ambalo ni hatari kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri na watembea kwa miguu.

“Jeshi la polisi liko makini katika kipindi hichi cha sikukuu ili kuhakikisha wananchi wanasherehekea sikukuu bila ya matatizo na linawaomba madereva kuachana na tabia ya kutumia vilevi ili kuepuka ajali wakati huu,” alisema Kamanda Matei.

Aidha alisema kuwa kikosi cha usalama barabarani kitahakikisha madereva wanafuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali ambazo zianweza kutokea na kuleta madhara kwa watu.

“Tunasisitiza madereva kuachana na ulevi wakati wa kuendesha kwani uzoefu unaonyesha ajali nyingi zimekuwa zikitokana na matumizi ya ulevi hivyo waache matumizi hayo na endapo watabainika watachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Kamanda Matei.

Kwa upande wa wananchi aliwataka kutumia ulinzi jirani kwa kuacha mtu au watu badala ya kuondoka wote na kuacha nyumba peke yake jambo ambalo linaweza likasababisha wizi majumbani.

“Wezi wamekuwa wakitumia mwanya wa kuiba kwenye nyumba ambazo hazina watu hivyo hata kama nyumba nzima imetoka ni vyema wakatoa taarifa kwa majirani ili wawalindie nyumba zao,” alisema Kamanda Matei.

Aliwataka wamiliki wa kumbi za starehe kutojaza watu kupita kiasi ili kuepuka athari ambazo zinaweza kujitokeza endepo watakuwa wamejaza watu wengi kwenye kumbi zao.

“Kuna hatari nyingi zinazotokana na kumbi kujaa kupita kiasi mfano watu kukosa hewa na kusababisha vifo au bahati mbaya shoti ya umeme endapo itatokea hivyo lazima wazingatie masharti ya leseni zao zinavyowataka ili kuepusha athari kama hizo,” alisema Kamanda Matei.

Alibainisha kuwa jeshi lake limejipanga kuhakikisha kuwa sherehe hizo zinafanyika kwa amani na utulivu kwa kuweka ulinzi kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya doria mitaani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 27, 2014

    "kuhimarisha" ndio mtaa gani? jamani kiswahili sijui kinaenda wapi?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...